ARUSHA MWENYEJI MASHINDANO YA FEASSSA
Jumanne, Juni 04, 2019
ARUSHA MWENYEJI MASHINDANO YA FEASSSA

MASHINDANO ya vyama vya michezo kwa shule za msingi na sekondari katika nchi za Afrika Mashariki (FEASSSA) yanatarajiwa kufanyika jijini hapa kuanzia Agosti 15 hadi 25.

Jumla ya wanamichezo 3,000 kutoka Kenya, Uganda, Burundi, Rwanda, Zanzibar, Sudan na wenyeji Tanzania watachuana vikali katika mashindano hayo.

 Akizungumza katika kikao cha mwisho mkurugenzi wa maendeleo ya michezo idara ya usimamizi wa elimu ofisi ya Rais -TAMISEMI, Leonald Thadeo alisema kikao cha mwisho walikutana na wajumbe kutoka nchi husika juu ya kufanya ukaguzi wa mazingira ya malazi na miundombinu kwa ujumla na kusema mpaka sasa maandalizi yako vyema.

 “Katika kikao hiki wajumbe kutoka nchi husika walishiriki na kwa upande wa Sudan hawakushiriki kikao hiki cha mwisho lakini wametuhakikishia watafika katika mashindano haya,”alisema Thadeo.

 Alisema michuano hii ni muhimu kwa nchi hizi kwani imeshaonesha kuzalishwa kwa vipaji ambavyo vinasaidia kuunda timu mbalimbali za taifa na kusema serikali ya mkoa kupitia ofisi ya katibu tawala wametoa ushirikiano mkubwa na kuhakikisha kuwa watatilia maanani usimamizi katika suala zima la ulinzi na usalama.

Habari Leo