Samia amwakilisha Magufuli Niger
Jumanne, Julai 09, 2019
Samia amwakilisha Magufuli Niger

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan ameshiriki katika Mkutano wa 12 wa Dharura wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Umoja wa Afrika kuhusu Mkataba wa Uanzishwaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA), unaofanyika jijini Niamey, Niger.

Akiwa katika mkutano huo, aliipongeza serikali ya Ghana kwa kuchaguliwa kuwa Makao Makuu ya Sekretarieti ya AfCFTA na kuisihi Kamisheni ya Umoja wa Afrika, kuharakisha ukamilishaji wa muundo, wa bajeti na mpango kazi wa Sekretarieti hiyo ili ianze kufanya kazi haraka.

Mkutano huo wa wakuu wa nchi na serikali umepokea taarifa ya Mahamadou Issoufou, Rais wa Jamhuri ya Niger kuhusu utekelezaji wa AfCFTA ambayo pia imepitishwa na viongozi hao.

Mkataba wa Uanzishwaji wa Eneo Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA) umeanza kazi rasmi Mei 30, mwaka huu na unahusu uasili wa bidhaa zitakazouzwa katika soko la Afrika, kufungua biashara ya bidhaa kwa asilimia 97 na uanzishwaji wa Sekretarieti ya kusimamia utekelezaji wa Mkataba wa AfCFTA.

Aidha, alimpongeza Rais wa Niger, Issoufou, kwa jitihada zake za kuhakikisha azma ya Umoja wa Afrika ya kuanzisha Soko Huru la pamoja la Afrika inafikiwa. Makamu wa Rais pia alizipongeza nchi 27 wanachama wa Umoja huo, zilizoridhia mkataba wa uanzishwaji wa Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA) kati ya nchi 54 zilizotia saini mkataba huo na kuahidi kwamba Tanzania itaungana nao baada ya kukamilisha taratibu za ndani.

Kwenye mkutano huo, Mama Samia alimwakilisha Rais John Magufuli ambapo alitoa salamu kwa niaba yake kwa wakuu wa nchi na Serikali waliohudhuria mkutano huo.

Gazeti la Habari Leo.