Serikali ya DRC yaidhinisha mpango wa elimu bure
Alhamisi, Septemba 05, 2019
Serikali ya DRC yaidhinisha mpango wa elimu bure

DRC. Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imeidhinisha mpango wa elimu bure katika shule za msingi za umma kwa lengo la kutekeleza yaliyomo kwenye katiba ya mwaka 2005 ambao inasisitiza elimu ya bure kwa watoto wa shule za msingi.

Tangu mwaka 1993, wazazi katika nchi hiyo wamekuwa wakiwalipa walimu ada ya mafunzo lakini sasa serikali imeamua kuwalipa mishahara walimu hao, hivyo wazazi hawatalipa ada tena.

Hata hivyo, baadhi ya walimu mpaka sasa wana mashaka kuhusu utekelezaji wa mpango huo mpya wa serikali. Walimu wanatishia kuanza mgomo ifikapo Septemba 20 ikiwa Serikali haitawalipa mishahara wa kutosha.

“Rais (Felix Tshisekedi) amechukua hatua hiyo ili wazazi wasilete tena pesa, sisi tumemuunga mkono, hapa nina walimu ambao hawajawahi kupokea pesa kutoka serikalini, nadhani ni muhimu kulipa walimu. Kama walimu hawatalipwa haraka, itakuwa na athari sana,” amesema Godé Moju ambaye ni mkurugenzi wa shule ya Kilimani iliyopo mjini Kinshasa.

Kwa mujibu wa shirika la habari la BBC, gharama ya elimu ya bure kwa watoto wa shule ya msingi ni takribani asilimia 40 ya bajeti ya nchi hiyo ambayo ni karibu Dola za Marekani sita bilioni.

Wachambuzi wa uchumi wana shaka iwapo hatua hio ya serikali itafanikiwa lakini Rais Tshisekedi ana matumaini makubwa.

Gazeti la Mwananchi.