Tanzania yaimarisha mipaka
Jumanne, Juni 11, 2019
Tanzania yaimarisha mipaka

MIPAKA ya Tanzania na nchi za Kenya, Uganda na Burundi imeanza kuimarishwa katika hatua mbalimbali ili kufikia lengo la serikali kuhakikisha ifikapo mwaka 2022 uimarishaji wa mipaka hiyo kuwa imekamilika.

Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi alibainisha hayo katika hotuba yake ya bajeti aliyoitoa hivi karibuni na kueleza kuwa katika Mwaka wa Fedha 2018/2019 wizara iliahidi kuendelea na uimarishaji wa mpaka wa Tanzania na Uganda, Tanzania na Burundi, Tanzania na Kenya na Tanzania na Zambia.

Aidha, uimarishaji huo unakwenda sambamba na katika mipaka ya nchi ndani ya Ziwa Tanganyika na nchi za Burundi, Zambia na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

Lukuvi alisema ununuzi wa vifaa vya ujenzi wa alama za katikati za mpaka umefanyika, maandalizi ya kuweka alama za mpaka yamefanyika kupitia kikao cha makatibu wakuu wanaohusika na mpaka wa Tanzania na Uganda kilichofanyika Aprili mwaka huu mjini Bukoba,mkoani Kagera.

Alisema mpaka ndani ya maji katika Ziwa Victoria kati ya Tanzania na Uganda wenye urefu wa kilometa 246 haujaanza kuimarishwa.

Aliongeza kuwa mpaka wa Tanzania na Kenya wenye urefu wa kilometa 819.7 kati ya hizo kilometa 760 za nchi kavu na kilometa 59.7 ziko ndani ya maji katika Ziwa Victoria. Uimarishaji wa mpaka huo unaelezwa kujumuisha utengenezaji wa ramani za msingi, kupima kipande cha mpaka na kusimika alama za ardhini.

Alisema kilometa 172 kati ya 760 za nchi kavu ziliimarishwa kufikia Juni mwaka jana na kwa mwaka wa fedha 2018/2019 mpaka mei mwaka huu kilometa 128 kutoka Ziwa Natron hadi Namanga zimekaguliwa ili kubaini mahitaji halisi.

Waziri alisema mpaka kati ya Tanzania na Zambia ni kilometa 345 ambapo sekta ya nchi kavu ina kilometa 289 na ndani ya maji ina urefu wa kilometa 56 maandalizi yanaendelea kwa ajili ya kuimarisha mpaka huo kwa makubaliano na Serikali ya Zambia ifikapo mwezi huu.

Gazeti la Habari Leo.