Uganda Airlines kupasua anga Tanzania, Kenya
Jumanne, Agosti 06, 2019
Uganda Airlines kupasua anga Tanzania, Kenya

NDEGE za Shirika la Ndege la Uganda (Uganda Airlines), zinatarajiwa kuanza kupasua anga la nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuanzia Agosti 28 mwaka huu.

Hiyo ni baada ya kupata cheti cha ruhusa (AOC) kilichotolewa kwa shirika hilo, kuruhusu kuanza shughuli zake.

Waziri wa Kazi na Usafirishaji, Monica Azuba amewaeleza waandishi wa habari kuwa shirika hilo litaanza safari zake ndani ya mwezi huu.

Litaanza na ndege zake mpya zilizonunuliwa na serikali hivi karibuni.

Kwa mujibu wa Azuba, shirika hilo litaanza safari zake katika miji ya Nairobi nchini Kenya, Dar es Salaam, Tanzania na Mogadishu nchini Somalia.

“Vituo hivi ndivyo tutakavyoanza navyo, baada ya hapo tunategemea kuongeza vituo vingine katika miji mingine ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki,” alisema waziri huyo.

Alisema baada ya kupata uzoefu wa kutosha katika miji hiyo mitatu, Uganda Airlines litaongeza idadi ya safari zake katika vituo na miji mingine ya Afrika Mashariki.

Baadhi ya miji ambayo inatarajiwa kuwemo katika nyongeza hiyo ni Kilimanjaro nchini Tanzania, Juba Sudan Kusini, Bujumbura Burundi na Mombasa nchini Kenya.

Waziri huyo alisema mara baada ya shirika hilo kuongeza ndege mbili mwezi ujao, shirika litakuwa katika nafasi ya kuongeza safari katika miji ya Kinshasa, Khartoum, Addis Ababa, Zanzibar, Kigali, Harare, Lusaka na Johannesburg.

Gazeti la Habari Leo.