Bandari Mtwara na fursa kiuchumi Kusini, nchi jirani
Jumanne, Novemba 26, 2019
Bandari Mtwara na fursa kiuchumi Kusini, nchi jirani

BANDARI ya Mtwara ni mojawapo kati ya bandari kuu tatu za mwambao wa bahari zilizopo nchini, zinazosimamiwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA).


Uwezo wa bandari hiyo kwa sasa ni kuhudumia kwa usalama meli zenye urefu wa mita 222 na kina cha maji kisichozidi mita 9.5 katika gati yenye urefu wa mita 385.


Akiizungumzia bandari hiyo, Meneja wa wake, Mhandisi Juma Kijavara, wakati akitoa taarifa ya utendaji wa kazi, anasema huwa inatumika katika kufanikisha biashara kwa bidhaa zitokanazo nchini kwenda nchi za nje ikiwamo Msumbiji, Comoro, India na Vietnam.


Anasema imekuwa ikihudumia zaidi shehena ya korosho ambayo ni zao kuu la biashara kwa mikoa ya Kusini.


“Bandari hii inahudumia pia shehena za saruji, bidhaa za vyakula, mitambo kwa ajili ya miradi mbalimbali pamoja na shehena ya majimaji ikiwamo kemikali na mafuta. Sambamba na huduma hizi pia imekuwa msimamizi wa bandari za Lindi na Kilwa,’’ anasema Kijavara.


Anasema katika kipindi cha mwaka 2017/2018 na 2018 /2019 shehena iliyohudumiwa ni tani 106,170 ambazo ni pungufu kwa asilimia 71 ya 363,287 tani zilizohudumiwa kwa mwaka 2017/2018.


“Kupungua kwa shehena iliyohudumiwa kulitokana na kutosafirisha shehena ya korosho pamoja na makaa ya mawe kama ilivyokuwa katika matarajio ya bandari.

 

Mhandisi Kijavara anasema kuwa katika kipindi cha mwaka 2018/2019 idadi ya meli zilizohudumiwa katika bandari hiyo zilikuwa 141 ikilinganishwa na meli 66 zilizohudumiwa mwaka wa fedha 2017 na 2018 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 113 na kwamba hiyo imetokana na kuongezeka kwa meli za mwambao.


Anabainisha kuwa kuna miradi mbalimbali ya maendeleo inayofanyika katika bandari hiyo ikiwamo mpango wa ununuzi wa vifaa vya utekelezaji, ujenzi wa miundombinu ya bandari kwa kuzingatia mpango mkuu na mpango mkakati wa mamlaka.


Pia aligusia miradi ya maendeleo ikiwamo mpango wa ununuzi wa vifaa vya utekelezaji, ujenzi wa miundombinu ya bandari kwa kuzingatia mpango mkuu na mpango mkakati wa mamlaka.


Anasema serikali ina mpango wa kupanua Bandari ya Mtwara kwa kujenga gati nne mpya na kuifanya kuwa ya kisasa kwa ajili ya kuhudumia shehena ya gesi, mafuta na mazao ya kilimo ukanda wa maendeleo wa Mtwara unaojumuisha mikoa iliyopo kusini na nchi jirani
za Malawi, Zambia na Msumbiji.

“Awamu ya kwanza ya utekelezaji inahusisha ujenzi wa gati la urefu wa mita 300 la kuhudumia shehena mchanganyiko, ambapo mkataba kati ya TPA na mkandarasi ambaye ni muunganiko wa kampuni M/s China Rwailway Construction Engeneering Group (CRCEG) na M/S China Railway Major Bridge Engeneering Group (CRMBEG) za nchini China.


“Mradi huu ulisainiwa Machi 4 mwaka 2017; ujenzi wa gati hili unatarajiwa kukamilika Machi 2020 na hadi sasa kazi ya usanifu imekamilika na kazi ya ujenzi inaendelea na imefikia asilimia 55,’’ anaeleza Mhandisi Kijavara.


Anasema mradi huu ukikamilika utaiwezesha Bandari ya Mtwara kuhudumia shehena nyingi zaidi takribani tani milioni moja.


Anataja mradi mwingine kuwa ni wa mita ya kupima mafuta unaotekelezwa chini ya ofisi ya Rais, unaofanywa na mkandarasi M/s Endress+Hauser ya nchini Uswizi akishirikiana na kampuni ya kizalendo ya BQ Constractors Ltd, kwa ujenzi wa ‘flow meters’ za Mtwara, Dar es Salaam na Tanga kwa thamani ya Euro milioni 17.


Anasema kwa upande wa Bandari ya Mtwara, mradi utahusisha ujenzi wa ‘skid’ mbili pamoja na ‘control room’ kwa ajili kupima mafuta ya diseli na petroli.


Anasema mradi ukikamilika utakuwa umeiwezesha bandari kutekeleza maelekezo ya serikali na itakuwa na uwezo wa kupima mafuta halisi yanayopitia bandari hiyo.


Akizungumzia bandari ndogo ya Kilwa, Lindi, Rushungi na Kisiwa/Mgao, anasema kumefanyika upembuzi yakinifu na uandaaji wa michoro ya awali kwa ajili ya uendelezwaji wake.


Anasema mamlaka inakusudia kufanya uwekezaji mkubwa wa upanuzi wa bandari za Lindi, Kilwa na Kisiwa/Mgao, mradi ulioanza August 2019 na muda wa mradi ni miezi 18 hivyo, unategemewa kukamilika Februari 2021 kwa thamani ya Sh milioni 732.392.


“Mradi huu ukikamilika utaifanya mamlaka kuwa tayari kuhudumia mizigo ambayo inatokana na utekelezaji wa mipango ya serikali wa kujenga kiwanda cha mbolea Kilwa pamoja na usafirishaji wa mizigo mbalimbali ya uvuvi wa kibiashara, kilimo na viwandani,’’


Anaeleza kuwa kwa kipindi kirefu bandari hiyo imekuwa ikitegemea shehena ya zao la korosho hivyo kufanya kuwa ya msimu, kutokana na changamoto hiyo bandari imefanya juhudi ya kupata shehena.


“Mamlaka ya bandari imempa punguzo la bei ya usafirishaji Kampuni ya Dangote, kwa ajili ya kusafirisha shehena ya saruji na makubaliano ni kusafirisha shehena tani 120,000 kwa mwezi.


“Pia mamlaka imeingia makubaliano na Kampuni ya Market Insight kwa ajili ya kusafirisha makaa ya mawe kutoka Mkoa wa Ruvuma kupitia Bandari ya Mtwara kwenda masoko ya nje na matarajio ni kusafirisha tani 70,000 za shehena ya makaa ya mawe kwa mwezi pindi usafirishaji huo utakapoanza,’’ anasema Mhandisi Kijavara.


Pia alizungumzia suala la mafanikio ya kiulinzi na usalama katika bandari hiyo, ambapo anabainisha kuwa wameingia katika mfumo wa ulinzi wa meli na bandari kimataifa (ISPS CODE COMPLIANCE) mwaka 2013.


Anasema mara baada ya kuingia katika mfumo huo bandari ilianza kufuata kanuni za kiulinzi zinazotambuliwa kimataifa hivyo, kuwezesha ulinzi kuimarika na kupata mafanikio yaliyopo sasa.


“Kutokana na mafanikio hayo, Bandari ya Mtwara ni miongoni mwa zilizofanya vizuri kiulinzi pamoja na kuwa eneo lenye changamoto ya kiusalama mpakani mwa nchi ya Msumbiji,’’ anasema Mhandisi Kijavara.


Kuhusu urasimishaji wa bandari bubu, Ofisa Manunuzi na Ugavi wa Bandari ya Mtwara, Abdilah Salim, anasema bandari hiyo imefanikiwa kuzitembelea na kuzitambua bandari 59 zilizopo katika pwani ya Mkoa wa Lindi na bandari 11 zilizopo katika Mkoa wa Mtwara.


Anasema tayari mapendekezo yamewasilishwa makao makuu kwa ajili ya hatua za kuzirasimisha bandari bubu za Mbuyuni, Kilwa Kivinje, Mchinga II, Songosongo na Rushungi, Mikindani, Kisiwa, Msimbati, Kilambo na Litembe Pwani.


Salim anasema kurasimishwa kwa bandari hizo kutasaidia kuweka uwiano sawa kati ya wafanyabiashara wanaotumia bandari kuu ambao wanalipa kodi na wale walio katika bandari bubu ambao hawalipi kodi inavyotakiwa na kuiingizia nchi hasara kwa kukosa mapato.


Anasema kuna hasara mbalimbali zinazotokana na kutumia bandari bubu ikiwa ni pamoja na kuwa njia za maambukizi ya maradhi kutoka eneo la nchi jirani na kuingia nchini, pia kuwa sehemu ya kupitisha dawa za kulevya na hata bidhaa feki, jambo ambalo linaendelea kutafutiwa ufumbuzi.

 

Gazeti la Mtanzania