Kofi Annan
Jumatano, Agosti 19, 2020
Kofi Annan

KOFI ANNAN ndiye Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuanzia mwaka 1996 - 2006. Katibu Annan na Umoja wa Mataifa kwa pamoja walipata Tuzo ya Amani ya Nobeli mwaka 2001.

Jana Agosti 18 ni siku aliyofariki kiongozi huyo, anayekumbukwa na mataifa mengi kwa kuhangaikia amani na maridhiano duniani.

Ndiye aliyekuwa mwanzilishi na mwenyekiti wa Kofi Annan Foundation na pia Mwenyekiti wa Elders, Shirika la Kimataifa lililoanzishwa na Rais wa Kwanza mweuzi wa Afrika Nelson Mandela.

Annan aliyefariki Agosti 18, 2018 akiwa na miaka 80, alizaliwa Aprili 1938 nchini Ghana na kuaga dunia Agosti 18, 2018 akiwa jijini Bern Uswisi. Alipoondoka UN mwaka 2006 alimwachia kijiti cha uongozi wa Umoja wa Mataifa Ban Ki-moon, ambaye naye amemkabidhi Antonio Guterres.

Annan alikuwa ni Mwafrika wa kwanza kuchaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, akihudumu mihula miwili kuanzia mwaka 1997 hadi 2006. Baadaye akaendelea kulitumikia shirika hilo kama mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Siria na kufanikisha kupatikana kwa suluhisho la amani la mzozo wa nchi hiyo.

MAMBO MAKUU

Kiongozi huyo aliyezaliwa mwaka 1938 huko Kumasi ambao sasa ni mji wa pili kwa ukubwa nchini Ghana, alikuwa ni pacha akizaliwa na dada yake aitwaye Efua aliyeaga dunia 1991. Mwaka 1962 alianza kufanya kazi UN huko Geneva, Uswis na kuendelea na utumishi hadi mwaka 1993 alipochaguliwa kuwa Mkuu wa Oparesheni za Kulinda Amani.

Kuanzia mwaka 1997 aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa saba wa UN na akaweka alama zisizofutika kwa kuwa kiongozi mashuhuri kwenye harakati za amani. Alikuwa mmoja wa washindi wa Tuzo la Amani ya Nobel mwaka 2001. Baada ya miaka 10 ya kazi mwaka 2006 aliondoka kwenye uongozi mkuu wa UN.

ALIYOYAHAMASISHA

Wakati wa kumbukumbu ya kifo chake, iliyofanyika mwaka jana , Katibu Mku wa UN Antonio Guterres, anasema Annan alisihi kila mtu asiwe mtazamaji katika maisha na kuongeza “alitutaka sote tuchukue hatua dhidi ya upendeleo, ukatili na umwagaji damu.”

Anamuelezea kuwa ni kiongozi aliyeutetea ushirikiano wa kimataifa kwa nguvu zote, alikuwa muumini wa UN na mfumo wa kimataifa unaofuatao kanuni.

“Na lazima niseme, kifo chake kinauma sana kwa sababu hivi sasa tunahitaji zaidi kuliko wakati wowote imani hiyo.” Anasema Guterres.

Mrithi wa Annan Ban Ki-moon ambaye alipokea kijiti cha kuongoza UN mwaka 2006 anasema: “Nina uhakika kadri miaka inavyokwenda, historia itaonyesha kuwa Kofi Annan alikuwa kiongozi wa kipekee.

Hakuwa na majivuno lakini alizungumza na kusikilizwa. Alikuwa kiongozi aliyeshika mambo ya zamani lakini alikuwa na dira thabiti ya kuziangazia siku zijazo.”

Aliendelea kummwagia sifa akisema kuwa ni kiongozi ambaye ameacha dunia ikiomboleza kifo chake lakini pia ameipatia mchango wa kipekee ambao utakuwapo daima na utaendelea kuhamasisha, amani, haki , maridhiano na upendo.

MALENGO YA MILENIA

Wakati wa uongozi wa Annan kama Katibu Mkuu wa UN viongozi wa dunia walipitisha malengo ya milenia yaliyofikia ukomo mwaka 2015 na alishinda Tuzo ya Amani ya Nobel.

Katibu Mkuu huyo aliongoza na kupeleka mbele haki za binadamu na ulinzi wa amani duniani kote kwa kusisitiza kuwepo, ofisi thabiti ya maadili na kutokuvumilia kabisa ukatili wa kingono dhidi ya wanawake na watoto na kuhamasisha maendeleo endelevu.

Malengo ya Maendeleo ya Millenia yalipaswa kufikiwa mwaka 2015, yakiwa ni jukumu la Umoja wa Mataifa lililokubaliwa na wanachama kupunguza nusu ya umasikini duniani, kutoa elimu ya msingi kwa watoto wote na kuondoa ubaguzi dhidi ya wanawake.

SULUHU KENYA

Baada ya uchaguzi Mkuu wa Kenya, zilizuka vurumai za kisiasa na kiongozi huyu wa UN alitoa mchango mkubwa kuleta mapatano nchini Kenya baada ya ghasia zilizofuatia uchaguzi mkuu wa mwaka 2007.

Aliunda Tume ya Usuluhishi na kuwashirikisha viongozi kadhaa wa Afrika akiwamo hayati Rais wa Awamu ya Tatu , Benjamin Mkapa pamoja na Mstaafu Jakaya Kikwete.

Afrika Mashariki inamkumbuka kwa juhudi na kuingilia kati uhasama nchini Kenya ili kuisaidia nchi hiyo isitumbukie kwenye ghasia zilizokuwa zinatokana na matokeo yasiyokubalika ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007.

KULINDA AMANI CONGO

Annan anakumbukwa kwa kusaidia bila kuchoka upatikanaji wa amani ya Congo DRC.

Ulinzi wa amani ya Congo ulifuatia kusainiwa kwa mkataba wa kuacha mapigano uliofanyika Lusaka Zambia Julai 1999 ukihusisha mataifa ya Congo, Angola, Namibia, Rwanda, Uganda na Zimbabwe na kuanzia hapo Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa likaunda kikosi cha ulinzi wa amani nchini Congo maarufu kama vikosi vya kulinda amani vya Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (MONUSCO) ambavyo hata sasa vinaendelea na ulinzi wa amani katika eneo hilo.

 

IPP Media