Kupima uzito si kigezo cha hali nzuri ya lishe
Jumatano, 21 Oktoba 2020
Kupima uzito si kigezo cha hali nzuri ya lishe

JAMII imetakiwa kutambua kupima uzito pekee, si kigezo cha kuwa na hali nzuri ya lishe, badala yake wazingatie uwiano kati ya uzito,kimo na urefu.

Hayo yalielezwa  jana na Ofisa Mtafiti Mwandamizi Lishe,Maria Ngilisho wakati wa maonesho ya wiki ya chakula duniani yanayofanyika mkoani Njombe kitaifa.

Alisema watu wengi wanapenda kupima uzito wakiamini uzito mkubwa, ni kigezo cha kuwa na hali nzuri ya lishe.

“Watu wengi wanapenda kupima uzito, uzito pekee sio kigezo cha kutosheleza kuashiria na hali nzuri ya lishe. Ili kupata hali halisi ya lishe ya mtu, tunatumia kipimo cha uwiano kati ya kimo,urefu na uzito ili kupata fahirisi (Body Mass Index – BMI),”alisema.

Alisema mtu anapopanga mlo ili uwe mlo kamili, lazima atumie angalau chakula kimoja kutoka kila kundi la chakula kati ya makundi matano ili aweze kujiweka vema katika suala la kuwa na lishe bora.

“Ushauri kwa kuwa Mkoa wa Njombe, ni moja ya mikoa inayozalisha chakula kwa wingi, basi  hawana budi wajenge mazoea ya kutumia elimu ya lishe wanayoipata ili wasiwe wanazalisha bila ya kupata faida ya kuboresha afya zao,” alisema.

Ofisa Lishe Mtafiti kutoka taasisi hiyo, Elizabeth Lyimo alielezea kuhusu mchezo wa karata za mlo kamili ambao lengo lake, ni kuboresha uelewa wa wananchi kuhusu mlo kamili kwa njia shirikishi na ya kufurahisha ili kuvutia washiriki kujifunza.

“Mtu yeyote anaweza kucheza mchezo wa karata za mlo kamili. Masuala ya chakula katika ngazi ya kaya yanatekelezwa kwa asilimia kubwa na wanawake, wanaume wamekuwa wakishiriki kwa kiwango kidogo, basi mchezo huu unawalenga zaidi wanaume wa rika zote ili wapate uelewaa wa kupanga mlo iwe katika kununua vyakula au kuandaa mlo kwa ajili ya familia,”alisema.

Mteknolojia Mwandamizi wa Maabara kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe, Juvenary Mushumbusi alisema taasisi ina maabara mahususi kwa ajili ya kufanya uchunguzi wa

kimaabara ili kuiwezesha kutekeleza na kufanikisha majukumu yake.

“Maabara hii ina vitengo vitatu, ambayo ni mabara ya kemia ya chakula (Food Chemistry

 Laboratory), kazi kuu ya maabara hii ni kufanya uchunguzi wa sampuli za chakula ili kubaini uwepo na wingi wa viinilishe kama vile, protini, wanga, mafuta, vitamini, madini na phytochemicals. 

Alisema kitengo hicho hufanya uchunguzi wa kubaini ubora na usalama wa chakula kama vile uwepo na wingi wa  sumukuvu, madini tembo, sumu kwenye mihogo (cyanide) na vikolezo (food additives)”alisema.

Alisema”maabara ya baiokemia (Biochemistry Laboratory)kazi kuu ya maabara hii ni kufanya uchunguzi wa  sampuli zinazochukuliwa kutoka kwenye mwili wa  binadamu ili kubaini viwango vya virutubishi au viashiria lishe mwilini (Nutritional Biomarkers) mwilini kwa mfano, vitamini, madini na elementi mbalimbali, mafuta na wingi wa damu”alisema.

Hata hivyo aliongeza kuwa maabara ya maikrobiolojia (Microbiology Laboratory)

kazi kubwa ya maabara hiyo ni kufanya vipimo maalumu vya kilishe kama vile folate na amino asidi kwa kutumia mbinu za maikrobiolojia.

“Maabara hii hupima vimelea vinavyo patikana kwenye chakula ili kubaini usalama na ubora wake kimikrobiolojia km vile uwepo wa vijidudu vinavyosabisha magonjwa kwa mtumiaji wa chakula au vile vinavyoashiria kuharibika kwa chakula au vinavyoashiria hali ya usalama wa maeneo,mazingira yanayuhusika na  utayarishaji,usindikaji wa chakula husika na baadhi ya vimelea, ni kama salmonella, e-coli,shigella na saureus,”alisema.

Mtanzania