NMB kushirikiana na serikali kukuza utalii
Jumanne, Desemba 17, 2019
NMB kushirikiana na serikali kukuza utalii

WAKATI ikielezwa kuwa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki zinazofi kiwa na Ziwa Victoria, zinapoteza karibu Dola za Marekani bilioni 60 kila mwaka kutokana na kutolitumia vyema ziwa hilo, Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais Dk John Magufuli, imekuja na mikakati kabambe itakayohakikisha inavuna mabilioni ya fedha katika ziwa hilo.

Nchi nne za Afrika Mashariki zinazotumia ziwa hilo za Tanzania, Uganda, Kenya na Rwanda, kwa ujumla zimekuwa zikiingiza kipato cha Dola za Marekani bilioni sita pekee kwa mwaka, kiasi ambacho kinaelezwa kuwa kidogo mno, ikilinganishwa na fursa zilizomo ndani ya ziwa hilo.

Kutokana na kutotumia vyema ziwa hilo, kwa sasa nchi za Afrika Mashariki zinazotumia ziwa hilo zinapoteza Dola za Marekani bilioni 60 kila mwaka. Kihistoria, usafiri wa majini pamoja na mtandao wa reli, vinachangia kwa kiasi kikubwa usafirishaji wa mizigo na abiria katika ukanda wa EAC.

Usafiri katika Ziwa Victoria ni muhimu katika maeneo ya Kati na Kaskazini kutoka Mombasa hadi Dar es Salaam kupitia Bandari za Kisumu, Port Bell na Mwanza.

Akizungumza katika mkutano wa pamoja wa mawaziri wa kuweka mikakati ya matumizi ya Ziwa Victoria katika programu za usafiri, uliofanyika wiki iliyopita Kampala, Uganda, Waziri wa Ujenzi na Usafirishaji wa nchi hiyo, Monica Azuba, alisema kuna mafanikio kidogo yaliyopatikana kwa miaka mingi katika matumizi ya ziwa hilo.

“Tumekuwa na mafanikio kidogo kwa miaka mingi kwa usafiri wa majini hususan katika Ziwa Victoria lenye fursa nyingi za salama tena wa gharama nafuu katika ukanda huu,” alisema.

Alisema ingawa kuna mafanikio kadhaa katika mifumo mingine ya usafiri kama barabara, reli na usafiri wa anga kwa miongo kadhaa, lakini kwa usafiri wa majini hali si ya kuridhisha.

Azuba alitoa mfano kuwa nchini Uganda sekta ya usafiri majini, imekuwa ikizorota kwa miaka 35 iliyopita.

Katibu Mkuu Wizara ya Miundombinu na Usafirishaji Kenya, James Macharia, katika kile kinachoonekana kutaka kujipanga kutumia vyema fursa zilizomo ndani ya ziwa hilo, alieleza umuhimu wa kuendeleza mitandao mingine ya mawasiliano kama barabara na reli kwani inaunganisha usafiri wa majini katika Ziwa Victoria.

“Huwezi kujadili maendeleo ya bandari bila kuangalia unafikaje kwenye hizo bandari, ni muhimu kuendeleza pia mtandao wa barabara na reli,” alisema.

Macharia alitaka nchi nyingine kama Burundi, Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kujumuishwa kwa sababu ni chanzo cha masoko katika nchi nne, zinazotumia ziwa hilo.

Mikakati ya Tanzania Katika kinachoonekana Tanzania imepania kukamata fursa hizo, serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Magufuli, imekuja na mikakati mbalimbali, ikiwamo kuboresha usafiri wa meli na miundombinu mingine ya usafiri inayounganisha na ziwa hilo ikiwamo ujenzi wa daraja la Kigongo-Busisi.

Mikakati hiyo pamoja na kuwa na lengo la kuondoa adha ya usafiri wa abiria na mizigo na wananchi, lakini pia kuiwezesha Tanzania kuvuna mabilioni ya fedha kila mwaka kutokana na huduma za usafiri na uvuvi katika eneo lote, linalofikiwa na ziwa hilo ambalo ni la kwanza kwa ukubwa Afrika na la pili duniani. Ujenzi wa meli mpya ya MV Mwanza Hapa Kazi Tu, unaendelea kwa kasi katika ziwa hilo na unatarajiwa kukamilika Januari, 2021.

Ujenzi huo unagharimu Sh bilioni 89.764 na mpaka sasa umefikia asilimia 43.74 na unatekelezwa na kampuni za ukandarasi za Gas Entec Company Limited na Kangnam Corporation za Jamhuri ya Korea kwa kushirikiana na Suma JKT. Kampuni hizo zimeshalipwa Sh bilioni 39.249.

Meli hiyo itakuwa na uwezo wa kubeba abiria 1,200, tani 400 za mizigo, magari makubwa matatu na madogo 20 na inatarajiwa kufanya kazi kati ya Bandari za Mwanza, Kemondo, Bukoba na Musoma pamoja na kwenda nchi jirani za Kenya na Uganda na hivyo kukabiliana na adha ya usafiri kwa wananchi na mizigo katika Kanda ya Ziw,a baada ya MV Bukoba kupata ajali ya kuzama majini mwaka 1996 na meli nyingine nne kuharibika.

Ujenzi wa chelezo unaofanywa na kampuni za STX Engine Company Ltd na Saekyung Construction Company Ltd, zote za Jamhuri ya Korea kwa gharama ya Sh bilioni 36.4 unaendelea katika ziwa hilo na umefikia asilimia 68 na wakandarasi wameshalipwa Sh bilioni 32.85 sawa na asilimia 90 ya fedha zote.

Ukarabati mkubwa wa meli za MV Victoria na MV Butiama, nao unaendelea kufanywa na kampuni za KTMI Co. Ltd ya Jamhuri ya Korea na Yuko’s Enterprises (EA) Co. Ltd ya Tanzania kwa Sh bilioni 27.71, ambapo mpaka sasa Sh bilioni 11.57 zimeshalipwa na kazi imefikia asilimia 65.

MV Victoria ina uwezo wa kuchukua abiria 1,200 na mizigo tani 200, wakati MV Butiama ina uwezo wa kuchukua abiria 200 na mizigo tani 100. Meli hizo zitakuwa zinafanya safari kati ya Bandari za Mwanza, Kemondo, Musoma, Bukoba na Nansio-Ukerewe.

Ofisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Huduma za Meli (MSCL), Eric Hamissi, alisema ujenzi wa chelezo na ukarabati wa meli hizo, ambao unafanywa kwa kiwango cha kuzirudisha kuwa meli mpya, unatarajiwa kukamilika Machi, 2020.

Alisema wiki iliyopita kuwa kwa miaka minne, serikali imewekeza Sh bilioni 152 katika usafiri kwa njia ya maji na ameahidi kuwa MSCL itafanya kazi kwa juhudi na maarifa, kuhakikisha uchukuzi kwa njia ya maji unaboreshwa ukiwamo mpango mkakati wa kuanzisha huduma za usafirishaji mizigo katika Bahari ya Hindi kati ya Dar es Salaam, Comoro, Madagascar, Shelisheli na maeneo mengine kwani wameweza kufufua meli nne kati ya 14 zilizoachwa na Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere.

Wiki mbili zilizopita Rais Magufuli aliweka jiwe la msingi la ujenzi wa daraja la Kigongo-Busisi, linalounganisha wilaya za Misungwi na Sengerema za mikoa ya Mwanza na mkoa wa Geita na litakuwa ndilo daraja refu kuliko lote katika ukanda huu Afrika Mashariki na Kati na la sita kwa urefu Afrika.

Daraja hilo litaunganisha barabara zinazoenda nchi jirani za Uganda, Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), hivyo litatumika kusafirisha mizigo kutoka Ziwa Victoria kwenda katika maeneo hayo, hivyo kuingiza mamilioni ya fedha.

Ujenzi wa daraja hilo,utagharimu zaidi ya Sh700 bilioni likiwa na urefu wa kilomita 3.2 likipita juu ya Ziwa Victoria. Daraja hilo pia litaunganisha barabara zinazoenda nchi jirani za Uganda, Rwanda, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

 

Habari Leo