TAHAJIA KATIKA KISWAHILI SANIFU
Jumamosi, 2 Januari 2021
TAHAJIA KATIKA KISWAHILI SANIFU

TAHAJIA kwa mujibu wa Kamusi la Kiswahili Fasaha iliyoandikwa na BAKIZA ni ‘herufi zinazounda neno kulingana na mfumo wa lugha fulani’. Nayo Kamusi Kuu ya Kiswahili iliyoandikwa na BAKITA inasema kuwa tahajia ni ‘mpangilio wa herufi katika kuunda maneno kwenye lugha kwa mujibu wa kanuni na tahajia zilizokubalika katika lugha inayohusika, uendelezaji wa maneno’.

 Kwa mujibu wa kamusi hizi tunapata mwongozo wa jinsi maneno yanavyotakiwa kuandikwa katika makala mbalimbali za magazetini, kwenye majarida, vitabu na maandiko mbalimbali yanayofikisha ujumbe kwa jamii, iwe ni kuelimisha, kuburudisha, kuonya n.k. Pamoja na mwongozo huu mzuri kumejitokeza tabia ya kutozingatia miongozo ya uandishi, uendelezaji wa maneno au tahajia ya baadhi ya maneno. Kutokuzingatia tahajia za baadhi ya maneno kunaweza kusababisha kukosewa kwa maana au maana iliyokuwa imekusudiwa na mwandishi kutokuifikia jamii au hadhira yake. Inavyoelekea baadhi yetu hatuna utaratibu wa kutaka kuhakikisha ikiwa tulichokiandika ndicho tulichokikusudia au la.

Tunachojali zaidi mradi ujumbe wangu nimeupeleka kunakohusika. Huwa hatujiulizi maswali yanayofuata, je, ujumbe umefika kama nilivyokusudia? Kuna upotoshaji wowote wa maana niliyoikusudia? Je, nilichokisema ndicho kilichotakiwa au kinyume chake? Kamusi ndizo hutumika kuwaongoza watumiaji wa lugha jinsi tahajia mbalimbali zinavyotakiwa kuwa. Hata hivyo, si watumiaji wote wa Kiswahili ambao huamua kutumia miongozo hiyo wakati wa kuandika kazi zao. Wengi wetu tunadhani kwa kuwa sisi ni wazawa wa lugha fulani basi tunaifahamu lugha hiyo vilivyo. Hata hivyo, kinyume chake ni ukweli kwamba si kila mzawa wa lugha atafahamu usahihi wa maneno yote pasi kuangalia miongozo iliyopo; yaani kamusi. Pamoja na umuhimu huu wengi wetu hatuna kawaida ya kuangalia kamusi ili kupata usahihi wa maneno mbalimbali. Kuna sababu mbalimbali zinazomfanya mtumiaji wa lugha kutokutumia nyenzo mbalimbali zitakazompa mwongozo wa jinsi ya kuandika maneno mahususi. Kwanza, ni kujiona kuwa mzawa wa lugha fulani hivyo, hakuna haja ya kurejea vitabu na maandiko mbalimbali kupata usahihi wa maneno, kutokuwa na miongozo hiyo, kutokana na sababu mbalimbali kama vile, kuwa mbali na eneo miongozo hiyo inakopatikana, huenda mhusika yuko nje ya ofisi, kituo cha kazi au yuko safarini. Mara nyingi wengi wetu huwa hatuna kabisa miongozo hiyo. Tatu, ni kutokuona umuhimu wa kutumia miongozo hiyo kwa uzembe tu. Tahajia ya Kiswahili sanifu inatutaka kuandika maneno kwa usahihi kama mifano inayofuata inavyoonesha.

 

 Pamoja na usahihi unaotakiwa kwenye mabano nimeonesha kosa ambalo lilijitokeza: Mazingira ambamo mu- inajitokeza. Kiswahili sanifu kinatutaka kuhakikisha kuwa mu- inapofuatwa na irabu au sauti a, e, i na o basi neno hilo halina budi kudondosha u na kuweka w badala yake. Lakini mu- itabaki kuwa mu iwapo inafuatwa na irabu u. Angalia mifano inayofuata ambayo pia makosa yake yameoneshwa kwenye mabano. Mu + amini – mwamini (muamini) Mu + alimu – mwalimu (mualimu) Mu + ana anga – mwananga (muanaanga) Mu + embe – mwembe (muembe) Mu + ekundu – mwekundu (muekundu) Mu + izi – mwizi (muizi) Mu + ito – mwito (muito) Mu + ongo – mwongo (muongo) – asiyesema ukweli Mu + ombaji - mwombaji (muombaji) Kama nilivyosema awali, Mu itabaki kuwa mu ikiwa neno linalohusika linaanza na u-: Mu + umba – muumba (mwumba) Mu + ujiza – muujiza (mwuujiza) Mu + umini (mwuumini) Kama ilivyoonyeshwa hapo juu maneno yaliwekwa kwenye mabano hutumiwa kimakosa na waandishi wa Kiswahili sanifu bila kujali usahihi wake ni upi. Kuna wakati waandishi wanaamua kutumia lahaja nyingine za Kiswahili badala ya kutumia Kiswahili sanifu ambacho ndicho kinachotakiwa kutumika katika maandiko mbalimbali. Baadhi ya mifano ambayo inatumika kwa makosa imewekwa kwenye mabano na neno sahihi halijawekwa kwenye mabano.

Angalia mifano inayofuata: Heshima (hishima) Hekima (hikima) Sheria (sharia) Desturi (dasturi) Muda (mda, mida) Hasa (haswa) Maneno yaliyomo kwenye mabano si sanifu; hivyo basi yasitumike katika maandiko rasmi kwa kuwa yanapotosha matumizi fasaha ya Kiswahili sanifu. Kwa kuwa Kiswahili ni Kibantu maneno yote ya kigeni hayana budi kufuata tahajia ya Kiswahili sanifu ambacho ni Kibantu, hasa katika maneo muhimu yanayofuata: Neno lolote lisiishie na konsonanti hata kama halitakuwa na matatizo katika utamkwaji wake.

 Baadhi ya mifano hiyo ni: Salamu (salam) Mtaalamu (mtaalam) Maalumu (maalum) Isipokuwa neno moja tu Rais litabaki na kuandikwa vivyohivyo Rais na halina budi kuanza kwa herufi kubwa kwa kuwa hatuandiki rais Magufuli bali tunaandika Rais Magufuli. Mwambatano wowote wa herufi mbili au zaidi za konsonanti uepukwe isipokuwa kwa mwambatano unaohusishwa na herufi m, n, sh, y, sh, chw, w na konsonanti zenye asili ya maneno ya lugha ya kigeni ambazo hazina matatizo ya utamkwaji kama vile: st, sk, kt, chw, shw na dh Baadhi ya mifano hiyo ni: Mmomonyoko, mnong’ono, mnyonge, mnywaji, kichwa, lishwa, stakabadhi trekta, hekta, stesheni, steki, sketi n.k. Uunganishaji wa maneno una umuhimu wake katika lugha yoyote. Katika Kiswahili sanifu, maneno yataunganishwa kwa kuzingatia maana inayokusudiwa na kwamba maneno yatatakiwa kuwa neno moja katika mazingira haya: Neno likiandikwa kwa kurudiwarudiwa, kosa limo kwenye mabano. Kwa mfano: Huohuo (huo huo), walewale (wale wale), mbalimbali (mbali mbali), ndogondogo (ndogo ndogo), mojamoja (moja moja), fukuafukua (fukua fukua) n.k. Uunganishaji mwingine ni katika urejeshi uliomo kwenye kitenzi au kifungutenzi, kosa limo kwenye mabano. Kwa mfano: Utakachoandika (utakacho andika), alichosema (alicho sema), watakapokimbia (watakapo kimbia).

 Aidha, maneno yanayofuata yataunganishwa: Yeyote (ye yote) - (mtu), yoyote (yo yote) (kitu), wowote (wo wote), lolote (lo lote), popote (po pote), vyovyote (vyo vyote), mwomwote (mwo mwote), chochote (cho chote). Tunanatakiwa kuunganisha maneno yoyote yenye maana tofauti yanapounda maana moja mpya yakitumika pamoja, kosa limo kwenye mabano. Kwa mfano: Mwana + michezo – mwanamichezo (mwana michezo) Mfanya + kazi – mfanyakazi (mfanya kazi) Mwendo + kasi – mwendokasi (mwendo kasi) Mwenda + pole – mwendapole (mwenda pole) Kifuta + machozi – kifutamachozi (kifuta machozi) Muhimu: Maneno mengine yanayoingia kwenye kundi hili ni: Mwenyekiti (mwenye kiti) Mwenyezi (mweny ezi) Tatizo lingine kubwa linajitokeza katika tahajia ni ukataji wa maneno katika Kiswahili sanifu. Ukataji wa maneno ni namna au mtindo ambao endapo nafasi haitoshi kwenye karatasi au kifaa chochote cha kuandikia; basi neno hilo halina budi kufuata misingi na kanuni za ukataji wa maneno. Misingi hiyo ni pamoja na:

Neno lenye asili ya Kibantu litakatwa kufuatana na silabi zinazoliunda neno hilo. Lugha za Kibantu silabi huishia na irabu. Kwa hiyo, herufi ya mwisho katika neno lililokatwa haina budi iishie na irabu (a, e, i, o na u). Ufuatao ni ukataji sahihi na usio sahihi kwenye mabano: Maneno ukataji wake ni ma-ne-no (man-en-o, manen-o); Kuvuta ni ku-vu-ta (kuv-ut-a, kuvut-a); ng’ombe ni ng’o-mbe (ng’-ombe, ng’om-be); nyumba ni nyu-mba (ny-umb-a, nyum-ba); mnong’ono huwa m-no-ng’o-no (mn-ong’-on-o, mnong’-ono) na kutembea ni ku-te-mbe-a (kut-em-bea, kutem-bea) Maneno yenye asili ya kigeni ukataji wake utazingatia urahisi wa kutamka silabi kuliko silabi mwishoni mwa neno au silabi. Kwa kanuni hii, neno lenye asili ya lugha ya kigeni litakatwa mwisho wa silabi hiyo hata kama silabi hiyo haitaishia na irabu. Kwa mfano: Labda lab-da Alfajiri al-fa-ji-ri Maktaba mak-ta-ba Kortini kor-ti-ni Ustaarabu u-sta-a-ra-bu Stakabadhi sta-kaba-dhi Stesheni ste-she-ni Pamoja na misingi hiyo miwili ya ukataji wa maneno ya Kiswahili, neno halitagawanyika litakapokuwa katika mazingira haya yanayofuata; ikiwa: Neno lina silabi moja, kwa mfano Na, si, ni, ya, cha, la, wa, pa n.k. Neno hilo ni finyazo ya maneno mengine, kwa mfano: BAKITA, TAKUKURU, TATAKI, BAKIZA n.k. Jina la mtu, kwa mfano: Gertrude, Lulu, Mwanamboka, Athumani, Rose n.k. Tarakimu, namba au idadi, kwa mfano: 6, 3, VI, 20, 50, 100, 900 n.k. Hata hivyo, sauti ‘m’ na ‘n’ zinaweza kuwa silabi; hivyo basi, zinapaswa kutengwa kama silabi kamili. Ufuatao ni ukataji sahihi na usio sahihi kwenye mabano: Mtu ukataji sahihi ni m-tu (mt-u); Mmoja ni m-mo-ja (mmo-ja), mboni ni mbo-ni (m-bo-ni); nta ni n-ta (nt-a). Makala haya yameangalia ni kwa jinsi gani waandishi wa Kiswahili sanifu wanavyokosea katika tahajia ya Kiswahili. Waandishi wa Kiswahili sanifu hatuna budi kuhakikisha kuwa tunaandika habari au taarifa maandiko yoyote kwa kutumia tahajia sahihi. Aidha, waandishi hatuna budi kufuata miongozo inayotolewa. Pia, tutumie kamusi ambazo zitatusaidia kupata tahajia sahihi panapohitajika.