Tanzania sasa ni mlaji chakula, si mhudumu wa chakula
Jumanne, Desemba 10, 2019
Tanzania sasa ni mlaji chakula, si mhudumu wa chakula

Hali kadhalika, kwa sababu ya kuuza madini ya tanzanite ghafi , nchi za India na Kenya ambazo zinayaongezea thamani, zinauza madini hayo yenye thamani kubwa zaidi ya Tanzania ambaye ndiye mzalishaji pekee wa tanzanite duniani!


Ni kwa mantiki hiyo, Serikali ya Awamu ya Tano ilikuwa sahihi kuanza kushughulikia masuala ya muhimu - mambo ya ndani zaidi ya mambo ya nje. Masuala ya ndani yaliyoshughulikiwa kwanza ili kuwezesha utekelezaji wa diplomasia ya uchumi wenye manufaa kwa Tanzania ni pamoja na: kuanzisha viwanda vya kuongeza thamani ya bidhaa zitokanazo na rasilimali tulizonazo; kuchapa kazi kwa bidii na kuboresha nidhamu kazini, kushughulikia migogoro ya ardhi; na mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi.


Aidha, masuala mengine yaliyoshughulikiwa ni kufanya mabadiliko ya sheria na mikataba ya biashara na uwekezaji ili nchi inufaike na rasilimali zake, na kujenga mazingira mazuri ya kuvutia biashara, uwekezaji, utalii misaada na mikopo.


Hii ina maana kujenga miundombinu ya kisasa ya usafiri, mawasiliano na nishati ya umeme, kuondoa vikwazo vya kikodi na visivyo vya kikodi, kupunguza urasimu, kuimarisha upatikanaji wa huduma za muhimu za afya, elimu na maji; kujenga nguvukazi yenye umahiri; kuimarisha mifumo ya kisera, kisheria na kitaasisi; na kuimarisha ulinzi na usalama.


Nani asiyejua mchango na umuhimu wa masuala hayo ya ndani kwenye kukuza na kuendeleza biashara ya kimataifa, uwekezaji, misaada na mikopo, utalii, kupokea teknolojia, mazungumzo, na utambulisho na ujenzi wa taswira ya nchi.


Wakiunga mkono mtazamo huo wanazuoni wengi wanaamini kwamba, japokuwa mataifa makubwa yanazungumzia kubadilisha sura ya mfumo wa kiuchumi wa dunia, kupitia Mashirika ya Kimataifa kama Benki ya Dunia (WB) na Shirika la Fedha Duniani (IMF), ni nyumbani kwa kila nchi ndipo vita halisi ya maendeleo ya kiuchumi inapiganwa na kushinda.


Kwa mfano, mauzo nje ya nchi yanategemea ziadi nguvu/uwezo wa ushindani wa bidhaa au huduma zake, na ushindani huo unategemea masuala mengi ya soko la ndani. Kwa maana hiyo, nchi inayotengeneza mazingira mazuri ya ushindani ndani ya nchi, itakuwa na uwezo mkubwa wa kuteka soko kwa kuuza bidhaa nyingi kwenye soko la dunia. Vivyo hivyo kwa vipengele vingine vyote vya diplomasia ya uchumi.


UMUHIMU WA KUJITEGEMEA NA UTEKELEZAJI DIPLOMASIA YA UCHUMI


Wanazuoni wengi wanaamini kwamba, Taifa ambalo halijajitegemea, bado lipo chini ya utumwa na halijapata uhuru kamili. Kujitegemea hakumaanishi kuwa na uwezo wa kufanya mambo yote mwenyewe, bali kuwa na uwezo wa kutekeleza miradi muhimu ya kiuchumi kwa mapato ya ndani. Hayati Mwalimu Nyerere alisema: “Nchi haiwezi kuwa na uhuru kamili kama inategemea misaada na mikopo kwa ajili ya maendeleo yake.”


Nchi inayojitegemea - tofauti na nchi ombaomba - inaingia uwanja wa kimataifa ikiwa na fursa sawa na mataifa mengine. Ina uwezo wa kuzalisha baadhi ya bidhaa muhimu kama chakula, na inaingia sokoni ikiwa na kitu mkononi cha kubadilishana tofauti na nchi ombaomba inayopokea kilichopo sokoni bila kujali madhara yake.


Kwa mfano, kuna wakati tulikuwa na uhaba wa chakula, tukapewa msaada wa mahindi na dumuzi - mdudu mharibifu wa mazao. Nchi ombaomba haichagui na haiwezi kusema HAPANA.

 

Gazeti la Habari Leo