Udhibiti mifumo ya maabara na matarajio makubwa ya tafiti za dawa/vipimo
Jumanne, 15 Desemba 2020
Udhibiti mifumo ya maabara na matarajio makubwa ya tafiti za dawa/vipimo

UFANYWAJI wa Tafiti na majaribio ya dawa ni sehemu muhimu zaidi hasa katika  maendeleo ya nchi za uchumi wa kati na chini kama Tanzania.

Hii huendana na ubora wa maabara ambazo zinatumika kufanya tafiti na vipimo ili kuleta manufaa kwa wananchi ambao mwisho wa siku ndio wanatumia matokeo hayo.

Hapa nchini Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba(TMDA)  ndio yenye jukumu  la kuhakikisha uimara na ubora wa bidhaa hizo ambapo  hayo yote hutoka katika upimaji unaofaa wa maabara.

Serikali inazingatia ukaguzi na uimarishaji wa maabara mbalimbali  ili kuweza kukidhi vigezo vinavyotakiwa. 

Katika kulibainisha  hilo MTANZANIA Jumapili limezungumza na Mkurugenzi wa Pharm R&D Lab kutoka Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi  shirikishi Muhimbili(MUHAS)  Prof Eliangiringa Kaale ambaye anaeleza ni jinsi ambavyo wanafanikiwa katika kupima uwezo wa maabara zilizopo kanda ya Afika Mashariki na Nchi zingine za Afrika.

Prof Kaale anasema lengo la kuanzishwa kwa maabara hiyo ni kutoa mafunzo kwa vitendo kwa wafanyakazi wa viwanda vya dawa na wanafunzi wanasoma famasia.

“Kimsingi kuna mambo mawili katika  maabara kuna kufanya formulation na kufanya majaribio ya dawa,tumeanzisha huduma ya kutoa upimaji wa umahiri kwa wachunguzi wa sampuli.

 “Tunafanya hivi  kama maabara kwenye kiwanda kuna uzalishaji wa dawa na  dawa hazijaachiliwa  sokoni na zinapimwa ili kuhakikisha kama zinakidhi vigezo ambapo kuna maabara ambayo inafanya kazi hizo. 

“Na pia maabara hizo ziko kwenye mamlaka ambazo zinadhibiti ubora kama TMDA, kwa hiyo sasa ili zile maabara zinazofanya uchunguzi  matokeo yake yaaminike lazima zioneshe kwamba wana umahiri wa kuchunguza kwahiyo hiyo ‘program ya professional testing’ ni  mpango mahususi onaopima ubora wa maabara katika kuchunguza sampuli,”anaeleza. 

Anasema upimaji umahiri huongeza kuaminika kwa maabara katika viwango tofauti tofauti vya upimaji wa sampuli.

“Tunachokifanya tunatengeneza sampuli ambazo tunajua ina kiasi gani, mfano paracetamol kuna vitu tunaongeza ambazo wao hawavijui kwahiyo tunawasambazia na tunawaandikia na ‘protocol’ jinsi ya kupima ile sampuli.

“Halafu wakimaliza wanatutumia matokeo kuwa kuna kiasi gani kwa kila formular iliyopo kwahiyo tunapokea matokeo ya maabara zote ambazo zimeshiriki na kufanya upambanuzi.

“Na  kuna jinsi ya kuwapima kigezo ikifika  kati ya 0 na mbili tunasema maabara hiyo ina uwezo yaani matokeo yake yanakubalika  kama ikifika  kati ya mbili na tatu matokeo yake yana uwalakini yakiangukia tatu na kuendelea  matokeo yake hayaaminiki tena,”anabainsha Prof Kaale. 

Anaongeza;“Tunafanya  kuwajaribu kwasababu tuna maabara kwaajili ya kutengeneza dawa na kwaajili ya kupima uwezo wa dawa  mfano kama paracetamol utakuta kidonge kina mill 500 na kama ukitengeneza  kidogo hicho maabara inaweza ikadanganya na wanaweza wasichunguze wakajaza tu matokeo kwasababu wameona hiyo mill 500.

Kwa mujibu wa Prof Kaale wanachokifanya kutengeneza vidonge vya dawa vinavyofanana katika umbo na zile ambazo zinatumika katika soko lakini wanapunguza au kuongezea vitu vilivyotumika katika kutengeneza dawa hiyo. 

“Kwahiyo sasa wao wanatakiwa kupima na waripoti kilichopo kwasababu mara nyingi maabara zingine wanaweza wasipime wakaandika tu matokeo  kwahiyo ndio lengo letu huwa tunawatega. 

 MAABARA ZINAZOFAULU ZAONGEZEKA

Kutokana na kufanya upimaji wa umahiri katika maabara Prof Kaale anasema hali hivyo imesababisha kuendelea kuongezeka kwa ubora wa maabara kila mwaka.

“Wakati tulivyokuwa tunaanza tuliliona hilo kwasababu walikuwa  hawajui tumebadilisha kiwango lakini sasa wameendelea kuwa bora, mwaka 2013 ukiangalia mwenendo sasa tuko mzunguko wa tisa  yaani maabara ambazo zinafaulu sasa zinaongezeka kila mwaka kila tukitoa mzunguko  walioripoti walikuwa  asilimia 57  sasa tuko kwenye asilimia 90.

“ Na kila tukifanya tukaona  changamoto tunawapa mafunzo kwa kupitia matokeo pamoja na kusema changamoto zao tunazijadili jinsi ya  kuzidhibiti kama njia ya kuimarisha ubora.

Anasema maabara wanazoangalia ni zile za kikanda za nchi za Afika Mashariki na nje ya Afrika Mashariki na mapungufu yote yaliyoripotiwa.

“ Lakini baada ya kuanzisha ukaguzi tangu 2013 hadi 2020 kumekuwa na mafanikio makubwa  na tunategemea kuwa hili ni zoezi endelevu kwamaana kwamba ukishafikia kutoka matokeo hautapimwa tena. 

“Mfano kama hizo maabara ambazo zinafanya uchunguzi kuna kiwango cha ISOL ambacho wanapimwa nacho ili uweze  kutimiza masharti ya viwango lazima ushiriki  katika upimaji wa umahiri ni kigezo kimoja wapo na  sisi pia tunaendelea kufanyiwa ufuatiliaji. 

Anasema licha ya  kupima umahiri wa maabara mbalimbali lakini pia wao wanafanyiwa tahimini na shirika la kitaifa la Viwango .

“Na sisi kama watoa huduma  tunatathiminiwa  na bodi nyingine ili  ioneshe kuwa na sisi huduma tunazotoa zinakidhi vigezo  tuliomba tufanyiwe tathimini  mara ya kwanza walikuja  wakatufanyia pre assessment wakabaini mapungufu ya kawaida.

“Wakatueleza sehemu ambazo tunatakiwa kufanyia marekebisho tukazichukua na kuzifanyia kazi mwaka mmoja tukawatumia ripoti wakawatuma watu waje tena kwa ajili ya tahimini ya mwisho,”anaeleza Prof Kaale.

CHANGAMOTO 

Anasema changamoto ni ushiriki mdogo wa maabara kutokana na kuwepo kwa maabara nyingi katika ukanda.

“Moja ni ushiriki  lengo letu ni kuwa na washiriki wengi kwa mfano ukanda wetu kuna maabara nyingi zaidi ya 20 hadi 30 zinazoshiriki kwahiyo mwamko wa ushiriki bado mdogo hivyo ni vyema maabara kushirikia ili kuongeza viwago vya ubora.

UBORESHAJI UDHIBITI MAJARIBIO YA DAWA

Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba(TMDA)katika kuhakikisha kuwa wanaendelea kuboresha huduma   imezindua mradi  utakaowezesha udhibiti wa majaribio ya dawa, ufuatiliaji wa watu watakaopata  madhara  wakati wa majaribio ya dawa na mifumo ya utafiti.

Akizungumza wakati wa Uzinduzi wa mradi huo,Mganga Mkuu wa Serikali Prof Abel Makubi anasema  mradi huo umehusisha taasisi saba za ndani na nje ya nchi na utaongeza kasi ya udhibiti.

“Tumekuja kuzindua  mradi ambao una lenga kuboresha mifumo ya udhibiti ya majaribio ya dawa na tafiti mbalimbali tunazofanya Tanzania ,mradi huu unahusisha taasisi saba  pamoja na TMDA tuna wenzetu wa NIMR,MUHAS,KCRI, ,mamalaka ya udhibiti wa dawa Zanzibar (ZAHRI)  na taasisi ya utafiti Zanzibar(ZFDA)na taasisi  ambazo ziko nje ya Tanzania  universti ya st Andrews ya Scotlenda.

“Ujumuishaji wa taasisi wa nchi zilizoendelea na zile ambazo hazijaendelea  ni utaratibu ambao upo chini ya mradi wa taasisi ya EDCTP unaotoa fedha  kwenye taasisi ya nchi zinazoendelea  na zilizopo Ulaya  katika kuweka mifumo thabiti ya dawa na tafiti mbalimbali.

“Kikubwa ni kuweza kuimarisha mifumo ya udhibiti wa majaribio ya dawa ,mifumo ya utafiti ,namna ya kusoma na kupitisha maombi mbalimbali ya  udhibiti wa majaribio ya dawa kabla ya kutumika nchini.

“Tunalenga pia Kuweka  mifumo mizuri ya kufuatilia wale ambao watapata madhara  wakati wanatumia dawa za majaribio huwa dawa  za majaribio unakuwa hufahamu kama ni salama au sio salama  hivyo unatakiwa kuweka mfumo ambao utahakikisha wale ambao wanapewa  dawa hizo wanabaki kuwa salama bila kupata madhara yoyote   kwa hivyo mradi huu utaboresha mfumo huo,”anasema Prof Makubi.

Anaeleza kuwa mradi huo utahusika katika kutoa mafunzo kwa wataalmu wa utafiti  na walioko katika mamlaka ya udhibiti ili kuwajengea uelewa zaidi.

“Serikali na vyombo vyake tunawapongeza TMDA na kuwahimiza  kuwa tafiti zote za ‘clinical trial’ zinaweza kudhibitiwa na kuwa na viwango vinavyotakiwa na mwisho wa siku ziweze kutoa  majibu yanayotarajiwa kama ni dawa iweze kusaidia mwanadamu kama vipimo  viweze kuonekana kugundua tunachokitarajia,”alisisitiza Prof Makubi.

ATAKA GHARAMA KUPUNGUA

Prof Makubi anatoa wito kwa TMDA   kuangalia gharama za kujisajili ili uweze kupata  majaribio hayo ya dawa na vipimo hasa kwa wanafunzi  wa elimu ya juu.

“Mliangalie hilo kuona jinsi gani mnaweza kutatua bila kubadilisha viwango vya tafiti suala hilo nalisisitiza tuwajengee uwezo watafiti wetu vijana kwasababu tunawategemea,”anasema Prof Makubi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa TMDA, Adam Fimbo  anasema tafiti zitakazofanywa na mradi huo zinalenga  kugundua  dawa au vipimo ambavyo vinaweza kutumika na mwanadamu.

“Ili utafiti ukamilike lazima kutumia hatua mbalimbali ili dawa kutumika au kutumia vipimo katika  mfumo huo tunaanza na watu wachache ambao wanajitolea na baadae dawa ikionekana  ina manufaa haina madhara ndio sasa inaingia hatua ya kuelekea mwishoni  kwa kuanza kutumia

“Lengo letu ni kuhakikisha TMDA  na vyombo vyake kupunguza kero moja wapo ya kero  kuchelewa kupata uthibitisho  ili mtu apewe kuwa kufanya majaribio ya dawa  inachukua hadi miezi mitatu lakini kwa hii inajenga mifumo itakayoenda haraka,”anasema Fimbo.

Mtanzania