Jinsi ya kuepuka makosa 5 ya kiutawala kazini
Jumamosi, Machi 23, 2019
Jinsi ya kuepuka makosa 5 ya kiutawala kazini

KAZI ni sehemu ya maisha yetu ya kila siku. Hiyo ni kutokana na ukweli kwamba, binadamu hutumia muda mwingi zaidi mahali pa kazi kuliko sehemu nyingine yoyote.

Maana yake ni kwamba, ikiwa utashindwa kuboresha mazingira yako ya kazi au kazi yako ikisababisha kukunyima amani maishani, basi kunakuwa na tatizo.

Kwa upande wa viongozi au watalawa makazini, nao hupata changamoto kubwa sana wanapokuwa makazini. Kumbuka kwamba, kuwa kiongozi au mtawala kazini, kwanza kutakuhitaji usimamie heshima yako na ubora wa kazi, vyote kwa pamoja.

Kwanza uheshimiwe lakini heshima isiwe chanzo cha kuharibika kwa kazi. Usisahau kuwa utapaswa pia kuhakikisha walio chini yako wanakuwa wenye furaha na wanapenda kufanya kazi na wewe. Kwa maneno mengine ni kwamba, wewe usigeuke kero au chanzo cha kuwafanya wasifurahie kazi yao.

Pamoja na yote hayo, unapaswa kusimamia utendaji kazi uwe wenye tija na faida. Katika hilo, jambo la kwanza kabisa unalopaswa kuzingatia ni kutatua matatizo ya wafanyakazi haraka na kwa karibu.  Katika mada hii nimekuandalia makosa yanayofanywa na wengi ambayo huharibu kazi.

KUDUMISHA HADHI YA KAMPUNI

Biashara yoyote ni ushindani, hata kama upo juu kwenye biashara, lakini lazima kama kiongozi ufikiri zaidi namna ya kuendelea kuifanya kampuni au ofisi yako kuwa juu.

Ushindani ni kama nguvu ya umeme, unakuangaza lakini wakati huohuo ni hatari. Unaposimamia timu yako usifikiri tu “Je, kanuni hii itafanya kazi haraka?” badala yake jiulize, “Je, kanuni hii inaweza kufanya kazi vizuri zaidi?”

Usiamini sana akili yako peke yako. Weka mkutano na timu unayoingoza, kusikiliza mawazo yao ambayo yatakuongoza kwenye kusimamia heshima na hadhi ya kampuni au biashara.

MLINGANYO WA KAZI KULINGANA NA UWEZO

Ni makosa makubwa kutoa kazi kubwa kwa mfanyakazi ambaye unatambua uwezo wake ni mdogo. Usiogopeshwe na ukubwa wa timu, ni bora kutoa kazi kwa timu kubwa ambayo itakuwa na matokeo mazuri na ya uhakika kuliko kutoa kwa mtu mmoja mwenye uwezo usiokidhi na akaharibu kazi.

Wapo mabosi wengine wanapenda utaratibu wa kuwapa watu kazi za majaribio, ni sawa lakini wakati ukimjaribu, uwe na uhakika kuwa siyo kazi ambayo unaitegemea iende kwa mlaji. Toa majaribio kwa kazi ambazo unajua siyo za ushindani.

KUTOFUATILIA MAJUKUMU

Pamoja na mambo mengine, kazi ya kiongozi ni kugawa majukumu na kuyasimamia. Bahati mbaya ni kwamba, wapo baadhi ya viongozi ambao ni hugawa kazi, lakini hawafuatilii kujua ‘feedback’ ya kazi hizo.

Kufanya hivyo kunaweza kusababisha makosa makubwa, ambayo kwa sababu hukufuatilia hutayajua na badala yake, viongozi wako wa juu watagundua na utaonekana hauna umakini katika kazi yako.

Kitendo hicho kinaweza kukuvunjia uaminifu kazini, ama ukaonekana uwezo wako umepungua na mwisho inaweza kuwa ni kufukuzwa kazi.

MIPANGO YA SIKU KWA SIKU

Wapo baadhi ya mabosi wakishatoa kazi, huishia hivyo. Akishaweka mipango yake huacha moja kwa moja kwa watekelezaji wengine bila kuhakiki mara kwa mara. Hayo ni makosa.

Kama kiongozi ni lazima utakuwa una majukumu mengi, lazima kutenga angalau siku mbili za kila wiki, japo kwa saa chache kuchunguza upya baadhi ya majukumu uliyotoa, mipango yako ya mbele uliyojiwekea na ubora wa kile ulichopanga kwa walio chini yako.

Binadamu tumeumbiwa kusahau. Ukiacha mambo yaende yenyewe, bila shaka siku moja utakuja kugundua umefanya makosa makubwa lakini kumbe ni kwa sababu hukufuatilia kwa karibu.

KUMINYA UHURU WA WAFANYAKAZI

Kamwe usiwe kiongozi muoga na usiyeamini akili za wenzako. Wape wafanyakazi wako uhuru wa mawazo. Toa kazi na maelekezo kidogo, ukiruhusu kila mmoja kufikiri na kufanya vile anavyoona akili yake inamuongoza.

Kazi yako ni kufuatilia tu baada ya ukamilishwaji wa kazi husika na siyo kukatisha tamaa. Pamoja na ubosi wako, wakati fulani unaweza kufanya makosa, hivyo siyo vibaya kuruhusu maoni ya unaowasimamia.

Ukitengeneza nidhamu ya uoga, kuna siku yanaweza kutokea matatizo makubwa uliyosababisha mwenyewe kwa kuminya uhuru wa unaowaongoza.

Kwa leo naomba niishie hapa, tutakutana tena wiki ijayo. Wako katika mafanikio, naitwa Athumani Mohamed, wasalaam.

Gazeti La Mtanzania