Eritrea
Jumatano, Januari 02, 2019
Eritrea

Jina

Jina la nchi limetungwa mnamo mwaka 1890 na wakoloni wa Italia kutokana na neno la Kigiriki "erythraîa" linalomaanisha “bahari nyekundu”. Hii ni kwa sababu Bahari ya Shamu iliitwa "Sinus Erythraeus" na mabaharia Wagiriki au “Mare Erythraeum” kwa Kilatini na Waroma wa kale – maana yake ni "bahari nyekundu" – kwa Kiingereza “Red Sea”.

Jiografia

Eritrea iko katika eneo la Pembe la Afrika na ina Bahari ya Shamu upande wa kaskazini mashariki. Kwa mchanga wa pwani uliyo eneo kame pahali pa kutega samaki ni Funguvisiwa vya Dahlak.

Eneo ambalo liko kwa milima kusini si kame vile, lakini hali ya hewa ni poa. Mlima wa juu zaidi ni Soira, ambao uko kati ya Nchi Eritrea, mita 3018 juu ya bahari.

Miji

Mji mkuu wa Eritrea ni Asmara na miji mingine ni kama vile mji wa bandari Assab kusini mashariki, na pia miji kama Massawa na Keren.

Eneo

Eritrea imegawiwa katika maeneo 6:

Kati (Maekel)
Anseba
Kisini ziwa lekundu (Debubawi-Keih-Bahri)
Kaskazini ziwa lekundu (Semienawi-Keih-Bahri)
Kusini (Debub)
Gash-Barka

Historia

Hadi karne ya 19 maeneo ya Eritrea yalikuwa sehemu ya Ethiopia.

Pwani ilikaa karne nyingi chini ya utawala wa Uturuki au baadaye Misri kama nchi zenye nguvu kwenye Bahari ya Shamu.

Historia ya Eritrea kama eneo la pekee jinsi ilivyopata uhuru mwisho wa karne ya 20 ilianza na ukoloni wa Italia.

Mwanzo wa ukoloni wa Italia

Mnamo Novemba 1869 kampuni ya biashara ya Kiitalia ya Rubattino ilinunua bandari ya Assab kutoka kwa sultani wa Afar. Ilikuwa inatafuta kituo kwa meli zake zilizoanza kupita katika bahari ya Shamu baada ya kufunguliwa kwa Mfereji wa Suez mwaka uleule.

Serikali ya Misri ilipinga mapatano hayo kwa sababu ilidai eneo lilikuwa chini ya amri yake. Makubaliano hayakufikiwa hadi 1882, serikali ya Italia ilipochukua moja kwa moja mali ya kampuni kama koloni lake la kwanza katika Afrika.

Tangu kuporomoka kwa utawala wa Misri nchini Sudan, baada ya vita vya Al-Mahdi, Misri ilijiondoa pia katika pwani ya kusini mwa bahari ya Shamu. Italia ilitumia nafasi hiyo na tarehe 5 Februari 1885 ilipeleka wanajeshi mjini Massawa na kuitangaza kuwa koloni lake.

Waitalia waliendelea kuunganisha maeneo yao ya Assab na Massawa. Baadaye walijaribu kupanua utawala wao kutoka tambarare za pwani hadi nyanda za juu zilizokuwa chini ya Dola la Ethiopia.

Negus Yohanne IV hakufurahia kufika kwa Italia kwa sababu aliamini ya kwamba Massawa iliahidiwa kwake baada ya kuwasaidia Wamisri kujiokoa mbele ya jeshi la Al-Mahdi. Hivyo upanuzi wa Italia katika nyanda za juu ulikutana na upinzani.

Tarehe 26 Januari 1887 jeshi la Waitalia 587 walioelekea kaskazini lilishambuliwa karibu na Massawa kwenye kijiji cha Dogali na kushindwa na Ras Alula aliyekuwa mtemi chini ya Negus ya Ethiopia. Waitalia walipaswa kuongeza wanajeshi 13,000 ili kuhakikisha utawala wao.

Koloni la Eritrea

Baada ya kumaliza mashindano na Ethiopia, Italia tarehe 1 Januari 1890 iliunganisha maeneo yake yote katika koloni lililoitwa Eritrea kufuatana na jina la kale "Bahari ya Eritrea".

Katika kipindi hiki cha utawala wa kikoloni Eritrea ilitokea kama jamii na eneo la pekee. Koloni la Eritrea liliunganisha maeneo matatu yenye tabia za pekee:

kanda la pwani lililokuwa na historia ndefu ya biashara na mawasiliano na Uarabuni ng'ambo ya Bahari ya Shamu
kanda la Sahel katika kaskazini-magharibi lililowahi kuwa sehemu ya Sudan
kanda la nyanda za juu liliwahi kuwa sehemu ya utamaduni wa Watigray Wakristo
Italia ilianzisha miradi ya kufanya Eritrea chanzo cha malighafi kwa ajili ya uchumi wa Italia. Kijiji cha Asmara katika nyanda za juu kilikuwa mji mkuu wa koloni na kupanuliwa kuwa mji kwa ajili ya walowezi Waitalia. Asmara ilipambwa na majengo mazuri ya kisasa.

Katika miaka ya 1930 idadi ya motokaa zilizoendeshwa Asmara ilishinda idadi ya magari ya binafsi mjini Roma. Urithi huo wa majengo umekuwa sababu ya kuingiza Asmara katika orodha ya Urithi wa dunia ya UNESCO.

Waitalia walipanga na kujenga miji mingine kama vitovu vya biashara, mabandari, vituo vya kijeshi au vya kiuchumi.

Idadi ya wakazi wote ilikadiriwa kuwa takriban 200,000 mwaka 1890. Idadi hiyo iliongezeka haraka kufikia zaidi ya 600,000 mnamo 1939. Mabadiliko makubwa yalitokea hasa katika nyanda za juu ambako walowezi Waitalia walianzisha mashamba yao na miji mikubwa zaidi ilijengwa.

Idadi ya wasemaji wa Kitigrinya iliongezeka kutoka asilimia 35 mwaka 1905 kuwa asilimia 54 mwaka 1939.

Mwisho wa vita kati ya vikundi mbalimbali na kupatikana kwa huduma za kiafya pamoja na kuongezeka kwa upatikanaji wa chakula, vyote vilichangia katika kuongezeka kwa idadi ya watu.

Kati ya mabadiliko makubwa ulikuwa ujenzi wa barabara na reli kati ya Massawa, Asmara, Keren na Agordat. Viwanda kadhaa vilianzishwa, pia migodi ya kuchimba mawe au madini.

Sehemu za Waeritrea waliingia katika maisha ya ajira ya kibepari. Hivyo maarifa ya wakazi wa Eritrea hasa katika nyanda za juu yalikuwa tofauti na wenzao katika Ethiopia yenyewe walioendelea kuishi chini ya utaratibu wa kikabaila. Waeritrea walisukumwa katika maisha ya kisasa na uchumi wa fedha.

Hadi mwaka 1940 Eritrea ilikuwa tayari na tabaka la wafanyakazi wa viwandani na katika miji pia tabaka la wasomi wenye elimu ya kisasa.

Baada ya Mussolini kushika serikali, siasa ya Italia ilibadilika. Wafashisti walidharau Waafrika na kuanzisha siasa ya ubaguzi wa rangi. Wenyeji walipewa tu shughuli duni kabisa katika utumishi wa serikali.

Italia ya kifashisti ilifanya mipango ya kulipizia kisasi mapigano ya Adowa ikiandaa vita dhidi ya Ethiopia. Vita vilianza mwaka 1935 kutoka ardhi ya Eritrea. Silaha mpya za Italia (zikiwemo za kikemikali) zilishinda jeshi la Negus, hivyo Ethiopia yote ikawa koloni la Italia kwa miaka michache.

Waitalia walishindwa katika Vita Vikuu vya Pili ya Dunia mwaka 1941, ambapo Waingereza waliteka Ethiopia pamoja na Eritrea.

Eritrea huru

Baada ya kura ya wakazi wa Eritrea kukubali karibu kwa kauli moja, uhuru wa nchi ulitangazwa tarehe 24 Mei 1993 na kukubaliwa kimataifa.

Tangu hapo nchi inaendeshwa na chama kimoja bila uchaguzi.

Awali uhusiano na serikali mpya ya Ethiopia ulikuwa mzuri, lakini baada ya miaka ya kwanza ulizorota.

Mwaka 1998 kulitokea vita kati ya Eritrea na Ethiopia vilivyokwisha na ushindi wa Ethiopia. Wanajeshi la kulinda amani la UM wanajaribu kutunza hali ya kutopigana.

Kiongozi wa EPLF, Isaias Afewerki, akawa Rais. Eritrea (EPLF or Shaebia), ikawa chama pekee kinachotawala Eritrea kwa sheria na kubadilisha jina People's Front for Democracy and Justice (PFDJ).

Mwaka 1998, vita vya mpaka na Ethiopia vilileta kifo kwa wanajeshi wengi kwa nchi zote mbili, na Eritrea uchumi wake ukafifia na wananchi wakahangaika sana. Umma wa nchi ukanza kuhama na uchumi kukosa maendeleo. Eritrea ni nchi moja ya Afrika ambapo kuna shida ya mabomu ya ardhi. Serikali ya Ethiopia iliwafukuza WaEritrea ambao waiishi Ethiopia ama watu waliokuwa na utamaduni wa Eritrea baada ya vita na Eritrea. Hii iliwaletea Waeritrea shida na uhamaji.

Hata baada ya kuonyesha maendeleo kidogo kwa uchumi na siasa, serikali ya Eritrea inanyanyasa magazeti na waandishi na pia watu kwa siasa. Serikali yenyewe hata haijaweza kuweka Katiba mpya na kuleta kura ya kidemokrasia.

Baadaye, serikali ya Eritrea imeweza kusisitiza desturi ya ukoloni wa Waitalia ambayo inadai Kanisa na Dini kujiandikisha kwa serikali na kupewa ruhusa wa kuhubiri. Dini zilizopewa ruhusa na serikali ni Kanisa la Kiorthodoksi la Eritrea, Kanisa Katholiki, Kanisa la Mekane Yesus (Walutheri) na Uislamu. Nyingine zote, hasa zenye itikadi kali zimebanwa kote nchini.

Vita vya Eritrea na Ethiopia viliisha mwaka 2000 kwa mashauriano yanayojulikana kama Mapatano ya Algiers. Mojawapo ya makubaliano lilikuwa kuanzisha Muungano wa kimataifa wa kuweka amani, ambao unajulikana kama Muungano wa Kimataifa wa misheni ya Eritrea na Ethiopia (UNMEE); Walinda amani 4,000 wa UM wamebaki kutoka mwezi Agosti 2004.

Makubaliano mengine ya Algiers yalikuwa kuanzisha usawazisho wa mwisho wa mpaka uliyobishaniwa kati ya Eritrea na Ethiopia. Komisheni iliyokuwa na madaraka kutoka kwa UM, iliyoitwa Komisheni ya Mpaka wa Ethiopia na Eritrea (EEBC), baada ya mashauriano mrefu, ilikata maamuzi ya mwisho mnamo Aprili 2002, lakini maamuzi yao yakakataliwa na Ethiopia.

Kutoka Oktoba 2005 bishano la mpaka bado limebaki kuwa swali, hata kama umakini na mkomo wa vita unaangaliwa kwa kazo.Wanajeshi wa kulinda amani wa UM wanajaribu kutunza hali ya kutopigana.

Siasa

Bunge la Taifa la viti 150, liliyotekezwa mwaka 1993 baada ya Uhuru, lilimchagua Rais wa sasa, Isaias Afewerki. Kura za nchi huwa zinapangwa na kupanguliwa.

Shina za taarifa madaraka za kutangaza habari kwa siasa za nyumbani Eritrea haziko; na Septemba 2001 serikali ilifunga vyombo vya habari vya binafsi, na watu wanaopinga serikali hufungwa bila kushtakiwa. Hii yote ni kutoka taarifa ya washufu wa ulimwengu, kama Waangalizi wa haki za Kibinadamu (Human Rights Watch) na Wakombozi wa Kimataifa (Amnesty International).

Mambo ya nje yanahusu vita na Ethiopia, Sudan na Jibuti. Baada ya wajumbe wa serikali ya Eritrea wa Idara ya mambo ya kigeni kuenda Sudan, ushirikiano umeanza kuwa wa kawaida. Bishano na Ethiopia bado ni wazo kubwa la chuki ambalo limemfanya Rais kuuambia Umoja wa Mataifa ichukue hatua. Uagizaji huu umeelezwa kwa barua kumi na moja za Rais.

Watu

Wakazi wa Eritrea walikadiriwa kuwa 6,380,803 mwaka 2014.

Makabila makubwa ni Watigrinya (55%) na Watigre (30%), ambao wote wawanazungumza lugha za Kiafrika-Kiasia.

Nchi haina lugha rasmi ili kuheshimu sawasawa lugha zote. Hata hivyo Kitigrinya, Kiarabu na Kiingereza vina nafasi za pekee.

Serikali inatambua rasmi Kanisa la Kiorthodoksi la Eritrea, Kanisa Katoliki na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri pamoja na Uislamu. Makadirio yanatofautiana: Wakristo kwa jumla ni 50-68%, Waislamu 36-48%.

Mwaka 2004 Idara ya taifa ya Marekani (U.S. State Department) iliamua kwamba Eritrea ni Nchi mahsusi ya kufuatiliwa (Country of Particular Concern, au CPC) kwa kufinya uhuru wa dini.