Rwanda
Alhamisi, Januari 03, 2019
Rwanda

Kwa maana nyingine za jina hili angalia Ruanda

Republic of Rwanda (ing.)
République Rwandaise (far.)
Repubulika y'u Rwanda (Kinyarwanda)
Jamhuri ya Rwanda (Kiswahili)
Bendera ya Rwanda Nembo la Rwanda
(Details) (Details)
Lugha rasmi Kiingereza, Kifaransa, Kinyarwanda, Kiswahili
Mji Mkuu Kigali
Serikali Jamhuri
Rais Paul Kagame
Waziri Mkuu Anastase Murekezi
Eneo km² 26.338
Eneo la Rwanda Kazembe km² 123.553
Idadi ya wakazi 11,262,564 (Januari 2015)
Wakazi kwa km² 445
Uhuru kutoka Ubelgiji 1 Julai 1962
Pesa Rwanda-Franc
Wimbo wa Taifa Rwanda nziza (Rwanda nzuri)
Rwanda katika Afrika
Ramani ya Rwanda
Rwanda (kwa Kifaransa: Le Rwanda; zamani pia "Ruanda") ni nchi ya Afrika ya Mashariki isiyo
na pwani kwenye bahari yoyote.

Imepakana na Uganda, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Burundi na Tanzania.

Rwanda ni mwanachama wa Umoja wa Mataifa na wa Umoja wa Afrika.

Yaliyomo
1 Jiografia
1.1 Miji
2 Wakazi
2.1 Makabila
2.2 Demografia
2.3 Lugha
2.4 Dini
3 Historia
4 Siasa
4.1 Serikali
4.2 Ugatuzi
5 Tazama pia
6 Marejeo
7 Viungo vya nje
Jiografia

Hali ya hewa mjini Kigali.
Rwanda huitwa nchi ya vilima elfu (kwa Kinyarwanda: Igihugu cy'Imisozi Igihumbi; kwa
Kifaransa: Pays de Mille Collines): ndivyo sehemu kubwa ya eneo lake inavyoonekana, hasa
magharibi.

Ni nyanda za juu na milima; sehemu kubwa ni mita 1500 juu ya UB. Milima kaskazini mwa nchi
inapanda hadi mita 4507 juu ya UB. Kutokana na urefu huo hali ya hewa haina joto kali.

Mpaka na Kongo ni hasa Ziwa Kivu ambalo ni mojawapo kati ya maziwa ya bonde la ufa la
Afrika ya Mashariki.

Mpakani kwa Kongo na Uganda ndiyo milima ya kivolkeno ya Virunga.

Huko kuna mazingira ya pekee duniani yenye sokwe wa milimani. Wako hatarini kuangamizwa
kutokana na uwindaji na upanuzi wa mashamba unaopunguza mazingira wanamoishi.

Miji
Miji mikubwa zaidi ndiyo: Kigali wakazi 745.261, Butare wakazi 89.800, Gitarama wakazi
87.613, Ruhengeri wakazi 86.685 na Gisenyi wakazi 83.623.(namba za Januari 2005)

Kigali ni mji mkuu wenye kiwanja cha ndege cha kimataifa na mahoteli makubwa.

Gisenyi ni mji kwenye ncha ya kaskazini ya Ziwa la Kivu mpakani kwa Kongo ukiwa jirani na mji
wa Goma. Kuna usafiri wa mashua kwenda Kibuye na Cyangugu.

Kibuye ni mji mdogo ufukoni mwa Ziwa la Kivu. Una wavuvi wengi, kituo cha watalii na nyumba
za kihistoria za wamisionari. Hadi mwaka 1994 Watutsi 250,000 waliishi katika wilaya ya
Kibuye, lakini tangu uangamizaji wa Watutsi katika vita vya wenyewe kwa wenyewe wamebaki
8000 pekee.

Butare ni kitovu cha utamaduni kusini mwa nchi chenye chuo kikuu.

Wakazi
Wakazi wa Rwanda ni zaidi ya milioni 11. Banyarwanda milioni 2 wako Uganda na wengi zaidi
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Makabila
Kwa kawaida vikundi vitatu hutajwa kuwa wakazi wa Rwanda ndio Wahutu, Watutsi, Watwa.
Lakini kuna tofauti kali kati ya mawazo kama vikundi hivyo ni makabila, mataifa ya pekee au
matabaka ya kijamii. Hali halisi wanatumia lugha ileile ya Kinyarwanda na wanafuata utamaduni
uleule.

Wanahistoria wengi wanasema ya kuwa Watwa walikuwa wakazi wa kwanza wakiwa wawindaji,
Wahutu ndio wakulima wa Kibantu waliopatikana kwa uenezi wa Wabantu katika Afrika ya Kati
na mababu wa Watutsi waliingia kama wafugaji kutoka kaskazini.

Watutsi walikuwa tabaka la kikabaila, pia mfalme alikuwa Mtutsi. Lakini wengine wanaamini ya
kwamba vikundi vyote vitatu vilijitokeza nchini si kama tokeo la uhamiaji mbalimbali lakini zaidi
kama matabaka yaliyotofautiana kikazi: wakulima, wavindaji na wafugaji waliokuwa pia askari
wa mfalme.

Wakati wa ukoloni Wabelgiji walihesabu mwaka 1931 wakazi wa nchi kama ifuatavyo: 84 %
Wahutu, 15 % Watutsi na 1 % Watwa.

Kabla ya uhuru vilitokea kwa mara ya kwanza vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya makabila
mawili makubwa viliyosababisha kupungua kwa Watutsi kutokana na mauaji na zaidi kwa
Watutsi kukimbilia nchi jirani. Mnamo 1990 asilimia ya Watutsi ilikadiriwa kuwa 9 - 10 %.

Vita vya wenyewe kwa wenyewe vya miaka ya 1990 vilileta uangamizaji mkubwa wa Watutsi.
Kati ya asilimia 75 hadi 90 za wakazi Watutsi waliuawa katika wiki chache za mwaka 1994.
Baada ya mwisho wa vita Watutsi wengi ambao wenyewe au wazazi wao walikuwa
wamekimbilia Uganda na Tanzania walirudi tena Rwanda.

Demografia
Kwa wastani kuna wakazi 300 kwa kilomita ya mraba ambayo ni msongamano mkubwa kabisa
katika Afrika. Karibu nusu ya wakazi ni watoto hadi umri wa miaka 14.

Wastani wa muda wa maisha ni miaka 40 pekee. Vita vimesababisha idadi kubwa ya wagonjwa
wa UKIMWI.

Lugha
Lugha ya taifa, lugha rasmi na lugha ya mama kwa Wanyarwanda wote ni Kinyarwanda
ambayo ni lugha ya Kibantu, mojawapo ya Niger-Kongo.
Mijini na sokoni Kiswahili kinatumika pia lakini si lugha asilia ya Rwanda.
Lugha rasmi tangu enzi za ukoloni ni Kifaransa. Tangu mwaka 1994 serikali mpya, iliyoongozwa
na Watutsi walioishi miaka mingi Uganda, imetumia pia Kiingereza kama lugha rasmi ya tatu.

Dini
Tazama makala Uislamu nchini Rwanda
Kadiri ya sensa ya mwaka 2012 wakazi wengi ni Wakristo, hasa Waprotestanti (49.5%) na
Wakatoliki (43.7%). Waislamu ni 2%.
Kwa sasa serikali inazidi kufungia maabadi. Miezi saba ya kwanza ya mwaka 2018, imefungia
tayari makanisa 8,000.

Historia
Tazama makala "Historia ya Rwanda"
Rwanda ilikuwa ufalme tangu karne ya 16 kwa jina la Rwanda Rugali.
Mwanzo wa karne ya 20 ilikuwa sehemu ya Afrika ya Mashariki ya Kijerumani na sababu ya
mzozo kati ya Ujerumani na Ubelgiji.
Baada ya Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia Rwanda ikawa chini ya Ubelgiji kama eneo lindwa.
Uhuru katika mwaka 1961 ulifika pamoja na vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya Wahutu na
Watutsi. Uhusiano kati ya vikundi hivi viwili uliendelea kuwa vigumu.
Kuuawa kwa rais Juvenal Habariyama mwaka 1994 kulisababisha mauaji ya watu karibu milioni
moja (walau 600,000) kati ya Watutsi, Watwa pamoja na Wahutu wasio na msimamo mkali.
Kikundi cha RPF chini ya Paul Kagame kiliingia kati na kuchukua madaraka.
Tangu ushindi wake wa kijeshi mwaka 1994 RPF ilianzisha serikali ya umoja wa kitaifa.
Mwaka 2003 palitokea uchaguzi wa kwanza.

Rwanda pamoja na Burundi zilijiunga na Kenya, Uganda na Tanzania kama wanashirika wa
Jumuia ya Afrika Mashariki kwa maendeleo muhimu katika elimu, afya, uchumi na mambo
mbalimbali. Mwaka 2017 bunge la Rwanda liliamua kufanya Kiswahili kuwa moja ya lugha rasmi
nchini.[1]

Vita vya Kongo vilivyokuwa na majeshi ya mataifa mbalimbali (Kivu Conflict) vilimalizika mwaka
2012.

Siasa
Serikali
Rais na mkuu wa dola ndiye jenerali Paul Kagame (RPF). Waziri Mkuu ni Anastase Murekezi.

Ugatuzi
Kuanzia mwaka 2006 kuna mikoa mitano inayogawanyika katika wilaya kadhaa:

Mkoa Jina la Kinyarwanda Makao makuu Eneo
(km2) [2] Wakazi
(sensa ya mwaka 2012)[3]
Kigali Umujyi wa Kigali Kigali City 730 1,132,686
Kusini Amajyepfo Nyanza 5,963 2,589,975
Magharibi Iburengerazuba Kibuye 5,883 2,471,239
Kaskazini Amajyaruguru Byumba 3,276 1,726,370
Mashariki Iburasirazuba Rwamagana 9,458 2,595,703