Josina Machel
Alhamisi, Februari 07, 2019
Josina Machel

Josina Machel ni mwanamke aliethubutu kuinua silaha dhidi ya utawala wa kikoloni wa Kireno. Aliwahamasisha wanawake wengine pamoja na wanaume kuingia vitani kudai uhuru katika eneo lijulikanalo sasa kama Msumbiji.

Josina Machel ni nani? 

Alizaliwa kwa jina la Abiathar Muthemba tarehe 10 Agosti 1945,  katika mkoa wa kusini wa Inhambane. Tofauti ya kawaida kwa mwanamke wa Kiafrika wa wakati huo, familia yake ilimhimiza kwenda shule, na mwaka 1956 alihamia mji mkuu kisha akaitwa Lourenco Marques ili kuhudhuria shule ya upili ya kiufundi. 

Huko Machel alishiriki katika makundi ya kisiasa ya wanafunzi na akawa mwanachama wa chama cha chini kwa chini cha Ukombozi wa Msumbiji, ambacho kinajulikana zaidi kwa kifupisho chake cha kireno, FRELIMO. Chama hicho kikuu cha kisiasa nchini Msumbiji, kiliasisiwa nchini Tanzania mwaka 1962 ili kupigania uhuru wa Msumbiji kutoka kwa utawala wa Kireno.

Josina Michael alichangiaje jitihada za kupatikana uhuru?

Alipokuwa na miaka 18, Josina Machel aliamua kukimbia Msumbiji ili kujiunga na vita vya ukombozi dhidi ya Wareno. Katika jaribio lake la kwanza alitekwa katika iliokuwa Rhodesia ya Kusini (sasa ni Zimbabwe) akarudishwa nyumbani kwao na kufungwa jela kwa miezi kadhaa. Katika jaribio la pili, aliweza kufikia makao makuu ya FRELIMO katika mji mkuu wa Tanzania, Dar es Salaam - safari ya kilomita 3,500.

Alipata mafunzo ya kijeshi na akapanda vyeo katika safu ya FRELIMO, na kuwa mkuu wa idara ya masuala ya jamii mwaka 1969 akiwa na umri wa miaka 24. Mwaka huo huo, alifunga ndoa na Samora Moises Machel, ambaye angeendelea kuwa Rais wa kwanza wa Msumbiji iliyo huru mwaka 1975. Lakini Josina  hakuishi na kushuhudia nchi yake ikikombolewa kutoka kwa Wareno. Baada ya kuugua ugonjwa hatari alifia Dar es salaam mwaka 1971.

Kwanini Josina Machel alikuwa mtu maarufu?


Kwa sababu ya kujitoa kwakwe kupigania uhuru - alikataa hata ufadhili wa kusoma nchini Switzerland, akipendelea kubaki nchi mwake na kupambana dhidi ya utawala wa kireno. Pia alipigania haki ya wanawake kushiriki katika mapambano ya ukombozi, kutoka kubeba silaha na kuwa wanasiasa.

Lakini hakuwa mwanamke pekee aliepigania uhuru?

Ni kweli kwamba wanawake wengine pia walijidhatiti katika  mapambano ya kivita.  Wengi wao walitiwa moyo na mafanikio ya Josina katika harakati za ukombozi. Siri inayomzunguka Josina Machel inatokana na mchanganyiko wa kujitolea kwake binafsi, kifo chake cha mapema, na kuolewa kwake na mwanaume ambae alikuja kuwa rais wa Msumbiji.  Ndiyo maana haishangazi kwamba jina la ukoo alilolibeba kwa miaka miwili ndiyo anakumbukwa nalo.

Ni upi urithi wa Josina Machel?

Urithi wa Josina Machel unaamshwa kila mwaka katika siku ya kumbukumbu ya kifo chake Aprili 7. Katika siku hii, Msumbiji huadhimisha Siku ya Taifa ya Wanawake, na kuheshimu ushiriki wake kwa haki sawa.